Aleksander Mashuhuri

Aleksander Mashuhuri (Mkuu)
Mfalme wa Masedonia
Aleksander jinsi alivyomshambulia mfalme Dario wa Uajemi kwenye mapigano ya Issos (mozaiki ya Aleksander mjini Napoli, Italia)
Kusimikwa336
Vyeo vingineMkuu wa shirikisho la Wagiriki, Shahanshah wa Uajemi, Farao wa Misri, Bwana wa Asia
.
WakeRoksana wa Baktria
Stateira wa Uajemi
Parysatis wa Uajemi
NasabaNasaba ya Masedonia
BabaFilipo II wa Masedonia
MamaOlimpia wa Epiros
Kichwa cha Aleksander, sanaa ya Kiroma, marumaru mnami karne ya 1/2 BK

Aleksander Mashuhuri (au Aleksanda Mkuu, kwa Kigiriki Μέγας Αλέξανδρος, inayoandikwa kwa alfabeti yetu Megas Aleksandros) aliishi tangu Julai 356 KK hadi tarehe 11 Juni 323 KK.

Mfalme wa Masedonia (336323 KK), anajulikana kama mmoja kati ya amiri jeshi waliofanikiwa kupita wote wengine katika historia ya dunia. Kabla hajafariki kwa umri wa miaka 33 aliteka sehemu kubwa ya dunia iliyojulikana na Wagiriki wa zamani zake, kuanzia Ulaya hadi Bara Hindi na Misri.

Aleksander, familia na utoto

[hariri | hariri chanzo]
Aleksander na farasi Bukefalos; sanamu ya bronzi ya John Steell ya 1884

Aleksander alizaliwa mwaka 356 KK kama mwana wa mfalme Filippo II wa Masedonia na malkia Olympias. Masedonia ilikuwa nchi katika kaskazini ya Ugiriki ya Kale na Wagiriki wengi waliwatazama Wamasedonia kama washenzi walio nje ya ustaarabu wa Ugiriki. Tofauti na Ugiriki ya Kale iliyokuwa jamii ya madola-miji Masedonia iikuwa jamii ya miji michache na watu wengi walioishi vijijini. Ilitokea katika karne ya 5 KK tu ya kwamba wanamichezo kutoka Masedonia walikubaliwa kwenye Michezo ya Olimpiki.[1].

Filippo II alibadilisha hali ya Masedonia kwa kuimarisha jeshi lake hasa kuanzisha mbinu mpya za kupanga wanajeshi katika vikosi vya phalanx vyenye mikuku mirefu sana na kuunda vikosi vya askari farasi wazito wailokingwa kwa nguo za chuma kifuani na kofia kinga. Kwa kutumia jeshi hili alishinda madola mengine ya Ugiriki na majirani upande wa kaskazini na kuupatia ufalme wake kipaumbele katika Ugiriki. Baada ya kuunganisha Ugiriki chini ya uongozi wake kwa upanga alilenga kushinda pia mioyo yao kwa kuanza vita dhidi ya Milki ya Uajemi iliyowahi kupigana vita na Wagiriki mara kadhaa. Alianza kutuma sehemu ya jeshi kwenda Asia Ndogo[2] iliyokuwa wakati ule sehemu ya Milki ya Uajemi.

Kuna masimulizi mengi kuhusu utoto wa Aleksander ambayo mara nyingi ni hekaya zilizobuniwa baadaye. Hadithi moja inayokubaliwa na wanahistoria ni kuhusu Aleksader kijana wa miaka 10 aliyejipatia farasi iliyombeba baadaye hadi Uhindini. Katika simulizi hii mfalme alitembelewa na mtu aliyetaka kuuza farasi. Farasi moja aliyependeza hakuweza kupandwa na mtu yeyote na mfalme alimkataa. Hapo Aleksander aliomba ajaribu kumpanda akafaulu. Sababu yake ni Aleksander alitambua ya kwamba huyu farasi aligeuka ghafla akikiona kivuli chake wakati mtu alitaka kumpanda. Farasi alinunuliwa na Aleksander alimwita "Bukefalos" [3] akamtumia katika miaka ijayo hadi Misri na Bara Hindi.

Filippo alimwajiri mwanafalsafa Aristoteli kuwa mwalimu wa Aleksander katika falsafa, sanaa na hisabati. Aristoteli alimpa mwanafunzi wake wa kifalme nakala ya muswada ya Ilias[4] na Aleksander aliibeba kwenye kampeni zake za kijeshi. Aristoteli alidai kama sehemu ya malipo yake ya kwamba mji wake wa nyumbani uliowahi kuharibika vitani na Filippo kujengwa upya na raia wake waliowahi kuuzwa kama watumwa wanunuliwe na mfalme na kupewa uhuru.

Uhusiano baina ya kijana Alesander na babake ulikuwa baadaye na matatizo kutokana na husiano za kimapenzi za mfalme kando la mamake Aleksander.

Mfalme wa Masedonia (336 - 335 KK)

[hariri | hariri chanzo]
Ufalme wa Masedonia wakati wa kifo cha Filippo II na Aleksander kuanzisha utawala

Mwaka 336 KK mfalme Filippo aliuawa na mlinzi wake. Aleksander kijana wa miaka 20 alitangaziwa mfalme mpya kwa msaada wa jemadari Antipater. Aliagiza kuuawa kwa maafisa wa babake waliosambaza uvumi kuwa Aleksander aliuwa ameshiriki jatika uuaji wa babake. Mwaka huohuo alikutana na mabalozi wa miji ya Ugiriki walioapa kumtii.

Mwaka 335 alipaswa kufanya vita na makabila ya kaskazini walioingizwa katika ufalme na babake na sasa waliona nafasi ya kuasi, akawashinda.

Wakati Aleksander alipigania vita katika kaskazini miji ya Wagiriki waliona nafasi ya kutafuta uhuru upya wakaasi. Wakazi wa Thebes waliwafukuza askari wa Kimakedinia katika mji wao. Aleksander alirudi Ugiriki moja kwa moja baada ya ushindi wake kwenye kaskazini akateka mji wa Thebes akaamuru nyumba zote zibomolewe isipokuwa hekalu na nyumba ya mshairi Pindar. Wakazi 6,000 walichinjwa na 30,000 kuuzwa kama watumwa.

Sasa miji mingine ya Ugriki ilishikwa na hofu na kusalimu amri. Aleksander aliwasamehe Wagiriki kwa sababu aliwahitaji kwa mipango yake ya vita dhidi ya Uajemi. Alithebitishwa kama kiongozi na jemadari mkuu wa shirikisho la Wagiriki.

Kampeni dhidi ya Uajemi (334–333 KK)

[hariri | hariri chanzo]
Njia ya Aleksander katika Asia Ndogo mwaka 334-333 KK

Wakati wa Aleksander Milki ya Uajemi ilikuwa milki iliyotawala eneo kubwa duniani. Wakati wa karne mbili zilizotangulia watawala wa Uajemi waliwahi kuvamia na kuteka Mesopotamia, Shamu, Palestina, Misri, Asia Ndogo pamoja na sehemu za Asia ya Kati. Walijaribu mara kadhaa kuvamia Ugiriki pia lakini waliweza kushindwa kwa matatizo. Katika Asia Ndogo walitawala miji minghi ya Kigiriki iliyokaa ng'ambo ya Bahari ya Aegean. Hivyo Filippo II aliandaa vita dhidi ya Uajemi kwa sababu alitaka kutumia vita dhidi ya maadui wa miaka mingi kuimarisha nafasi yake kati ya Wagiriki. Uvamizi wa kwanza wa Masedonia katika Asia Ndogo ulirudishwa nyuma na Waajemi.

Aleksander alivuka mlangobahari wa Dardaneli katika Mei 334 akiwa na jeshi la askari 35,000 Wamasedonia na Wagiriki. Alimwacha jemadari yake Antipater huko Ugiriki na askari 12,000. Mfalme wa Uajemi alikuwa Darios III aliyesita kumpa jemadari moja mamlaka ya vita akaacha kazi hii kwa makabaila Waajemi katika Asia ndogo. Upande wa Uajemi kulikuwa pia na jemadari Mgiriki Memnon aliyemhudumia mfalme wa Uajemi kama askari wa kukodiwa. Alishauri kutomshambulia Aleksander vikali badala yake kumvuta ndani ya Asia Ndogo na kuharibu akiba zote za chakula anakoenda. Lakini Wakubwa Waajemi walikataa wakatafuta mapigano.

Mkutano wa kwanza wa Aleksander na jeshi la Uajemi ulitokea kwenye Mapigano ya Granikos[5]. Viongozi Waajemi walipanga jeshi lao vibaya wakapigwa na Wamasedonia.

Alesander aliendelea kupita kwenye miji ya pwani iliyokaliwa na Wagiriki na kumfungulia milango yao. Kwa njia hii alitaka kuondoa nafasi ya bandari kwa meli za nevi ya Waajemi zilizokuwa hatari kwa Ugiriki. Aleksander aliteua viongozi wenyeji kama maliwali wake katika majimbo ya Asia Ndogo na hivyo kuimarisha utawala wake.

Baada ya kumaliza miji ya pwani akaingingia ndani ya Asia Ndogo hadi Frygia. Hapa katika mji mkuu wa kale wa Gordion alikata fundo mashihuri wa Gordion. Kwenye ikulu ya kale mjini Gordion ilitunzwa gari la farasi la kale sana. Lilifungwa kwa kamba zilizopigwa fundo imara kupita kiasa. Ilisemekana kuna utabiri kuwa kama mtu angeweza uondoa fundo hili atakuwa mtawala juu ya Asia. Kutokana na hekaya ya kale Aleksander alitazama fundo akaiona gumu akatoa upanga wake na kuikata.

Kuelekea mwisho wa mwaka 333 Aleksander alipokwa habari kuwa mfalme wa Uajemi alikaribia Asia Ndogo kwa jeshi kubwa. Aleksander alipiga mbio kukutana naye. Kwenye mapigano ya Granikos mnamno 5 Novemba 333 majeshi ya Waajemi na Wagiriki yalikutana, tena ushindi ulikuwa upande wa Aleksander. Mfalme Dareios aliweza kukimbia kwa muda.

Mitazamo juu yake

[hariri | hariri chanzo]

Katika vitabu vya deuterokanoni vya Biblia anatajwa katika vitabu vya Wamakabayo kama mwanzilishi wa dola lililoeneza ustaarabu wa Kigiriki hata kuhatarisha imani ya Wayahudi na kuwadhulumu wakati wa mwandamizi wake Antioko Epifane wa Syria.

Katika kitabu cha Kizoroastria cha kipindi cha kati ya Uajemi kilichoitwa Arda Wiraz Nāmag Aleksander anajulikana kama “Aleksander aliyelaaniwa” kwa sababu alishinda milki ya Uajemi na aliangamiza mji mkuu wake ulioitwa Persepolis. Lakini katika habari za baadaye za Uajemi, mpaka Irani ya siku hizi, anaitwa Eskandar na hata alishangiliwa wakati Ukuta Mkuu wa Sadd-e Eskandar ulijengwa wakati wa Ufalme wa Parthia.

Pia anajulikana katika desturi za Mashariki ya Kati kama Dhul-Qarnayn kwa Kiarabu na Dul-Qarnayim kwa Kiyahudi na Kiaramu, yaani "mtu mwenye pembe mbili", huenda kwa sababu picha kwenye sarafu za wakati wa utawala wake ilimwonyesha kama anazo pembe mbili za kondoo dume za mungu Ammon wa Misri.

Jina lake kwa Kihindi ni Sikandar, neno ambalo ni sawa na “mtaalamu” au “mtu stadi.”


  1. Kwenye Michezo ya Olimpiki ya Kale ni Wagiriki pekee walioruhusiwa. Wamasedonia walikubaliwa kwa sababu mfalme wao alieleza ya kwamba alikuwa na mababu Wagiriki
  2. Eneo la Uturuki ya leo
  3. gir. Βουκέφαλος , maana yake "mwenye kichwa cha ng'ombe"
  4. Ilias ni kitenzi mashuhuri cha mshairi Homer kinachosimulia historia ya kale ya Ugiriki kwa mfano wa vita ya Troia
  5. Leo: mto Biga , mapigano yalitokea karibu na mji wa Biga katika Uturuki ya leo upande kusini wa Bahari ya Marmara.

Matoleo ya matini za kale

[hariri | hariri chanzo]
  • Arrian (1976). de Sélincourt, Aubrey (mhr.). Anabasis Alexandri (The Campaigns of Alexander). Penguin Books. ISBN 0-14-044253-7. {{cite book}}: Invalid |ref=harv (help)
  • Quintus Curtius Rufus (1946). Rolfe, John (mhr.). History of Alexander. Loeb Classical Library. Iliwekwa mnamo 28 Aprili 2015. {{cite book}}: Invalid |ref=harv (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Siculus, Diodorus (1989). "Library of History". CH Oldfather, translator. Perseus Project. Iliwekwa mnamo 14 Novemba 2009. {{cite web}}: Invalid |ref=harv (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Plutarch (1919). Perrin, Bernadotte (mhr.). Plutarch, Alexander. Perseus Project. Iliwekwa mnamo 6 Desemba 2011. {{cite book}}: Invalid |ref=harv (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Plutarch (1936). Babbitt, Frank Cole (mhr.). On the Fortune of Alexander. Juz. la IV. Loeb Classical Library. ku. 379–487. Iliwekwa mnamo 26 Novemba 2011. {{cite book}}: Invalid |ref=harv (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Trogus, Pompeius (1853). Justin (mhr.). "Epitome of the Philippic History". Rev. John Selby Watson, translator. Forum romanum. Iliwekwa mnamo 14 Novemba 2009. {{cite web}}: Invalid |ref=harv (help)CS1 maint: date auto-translated (link).

Kujisomea juu ya Aleksander na dunia yake

[hariri | hariri chanzo]

Kujisomea zaidi

[hariri | hariri chanzo]
* Badian, Ernst (1958). "Alexander the Great and the Unity of Mankind". Historia. 7: 425–444. {{cite journal}}: Invalid |ref=harv (help) 

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
* Delamarche, Félix (1833), The Empire and Expeditions of Alexander the Great.