Choo

Choo cha maji cha kukalia chenye kiti kilichopambwa

Choo (pia: msala) ni mahali ambako watu hutoa kinyesi, yaani mkojo na mavi. Neno hili latumiwa pia na watu kwa kutaja kinyesi, hasa wakilenga kuepukana na majina husika.

Kusudi la choo

[hariri | hariri chanzo]

Kinyesi huwa na harufu iliyosikiwa kuwa mbaya kwa hiyo watu hukiangalia kwa unyarafu. Kuna wataalamu wanaofikiri ya kwamba hali ya kusikia harufu ya mavi kuwa mbaya ni kutokana na hatari ya kiafya kutokana kinyesi hiki kwa wanadamu wenyewe. Mavi huwa mara nyingi na bakteria ndani yake zinazoweza kusababisha magonjwa kwa hiyo uwezo wa kusikia mavi kuwa na harufu mbaya na unyarafu dhidi yake ni kinga asilia dhidi ya maambukizo. [1].

Hapo tangu mwanzo watu hawakuacha kinyesi mahali pa kulala au kukaa. Mbinu iliyotumiwa ambako watu ni wachache katika mazingira asilia ni kwenda mahali pa mbali kidogo na kuacha kinyesi pale. Tangu watu kukaa pamoja katika vijiji au hata miji mbinu hii haikupatikana tena na hivyo watu walianza kubuni njia mbalimbali na kujenga vyoo.

Historia ya choo

[hariri | hariri chanzo]
Vyoo vya umma kutoka enzi ya Roma ya Kale mjini Ostia Antica, karibu na Roma, Italia
Chumba cha choo nje ya ukuta wa boma la Kampen, Ujerumani
Ndoo ya choo kwa matumizi katika migodi, mnamo 1930

Hatari ya kumwaga kinyesi katika mazingira ya makazi ilitambuliwa mapema jinsi inavyoonekana katika amri iliyohifadhiwa katika Biblia, kitabu cha Kumbukumbu la Torati 23,12 [2]

"Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje; nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho"

Akiolojia ilikuta vyoo vya maji katika miji ya kale huko Uhindi, China na penginepo. Katika mji wa Mohenjo-Daro katika bonde la mto Indus nyumba zilikuwa na vyumba vya choo vilivyotengenezwa kwenye ukuta wa nje; watu walikalia kwenye ya viti vilivyojengwa kwa matofali na kinyesi kilianguka katika nafasi iliyokuwa wazi upande wa nje ambako kilikusanywa na watumishi, vyoo vya aina hii vinapatikana hadi huko Afghanistani ambako kinyesi kinatumiwa kama samadi kwenye mashamba na mabustani nje ya miji. Nyumba nyingine katika Mohenjo-Daro zilikuwa na mabomba ya matofali ya kuchomwa yaliyopeleka majichafu nje ya nyumba.

Katika miji ya Roma ya Kale kulikuwa na vyoo vya umma ambako watu walikalia kwenye viti vilivyokatwa kwa mawe na chini yake maji yalipita na kupeleka kinyeshi katika mfereji chini ya ardhi hadi mto. Mji wa Roma ulikuwa na mfereji mkubwa uliofunikwa kwa matofali na mawe wa umbo la kuba na kukusanya maji machafu kutoka vyoo na bafu za umma na kuyapeleka hadi mto Tiber. Vyoo kwenye nyumba za Roma ya Kale kwa kawaida zilitegemea mashimo marefu chini ya nyumba.

Mahali pengi ya dunia watu walitegemea ndoo au sufuria za pekee ambazo walitumia kama choo na yaliyomo yake yalibebwa nje ya nyumba na kumwagiwa mahali palipofaa. Mbinu iliyotumiwa zaidi mjini ulikuwa shimo chini ya nyumba au, kama nafasi ilikuwepo, nje ya nyumba ambako jengo dogo lilikaa juu ya shimo la choo.

Katika karne ya 19 miji ya Ulaya ilikua haraka kutokana na mabadiliko ya mapinduzi ya viwandani na kuongezeka kwa watu pasipo vyoo vya kutosha kulisababisha kusambaa kwa magonjwa ya kuambukiza kama kipindipindu. Katika sehemu nyingi maji machafu yalitiririka katikati ya barabara katika mifereji isiyofunikwa. Kuongezeka kwa watu kulisababisha ndani ya ardhi kuchanganya kwa majichafu ya mashimo na maji ya visima. Maendeleo ya kisayansi yalileta elimu ya kwamba maambukizi yanapitishwa hasa kwa maji machafu si kwa hewa chafu jinsi ilivyoaminiwa awali. Hapo serikali zilianza kuweka taratibu za kujenga mifumo ya kukusanya majichafu, hasa kwa kutengeneza mifereji iliyofunikwa au mabomba ya kukusanya majichafu ya kila nyumba na kuyapeleka nje ya miji au hata penye vituo vya kusafisha majichafu kabla ya kuyarudisha katika mito. Mji mkubwa uliotangulia hapa ulikuwa London katikati ya karne ya 19.

Kukua kwa miji katika nchi za Afrika kumerudisha matatizo yaliyokuwepo mahali pengine pa dunia. Kuzidi kwa watu katika mitaa ya vibanda, kumwagika kwa kinyesi katika njia za umma na kuchafuka kwa njia za maji chache zilizopo karibu na makazi huongeza hatari ya maambukizo na kwa afya ya wakazi.

Hadi leo (mwaka 2015) takriban bilioni 2.4 za wakazi billioni 7.3 dunia wanakosa vyoo sanifu, na karibu bilioni 1 wanatoa kinyesi mahali pasipo na choo chochote[3].

Aina za vyoo

[hariri | hariri chanzo]
Choo cha maji chenye bomba la "S" linaloziba nafasi ya kuenea kwa harufu mbaya
Choo cha kuchuchumaa katika treni nchini Vietnam

Kwa jumla kuna aina mbili za kimsingi za vyoo ama vyoo vinavyotumia maji na vyoo visivyotumia maji.

  • Kazi ya maji kwenye choo ni kuhamisha kinyesi kutoka sehemu kinapoanguka na pia kufunga mabomba kinaposafirishwa na hivyo kuzuia harufu mbaya pamoja na nafasi ya bakteria kuzunguka.
  • Vyoo visivyotumia maji mara nyingi ni choo cha shimo lakini kuna pia vyoo vyenye teknolojia mbalimbali

Vyoo vya maji

[hariri | hariri chanzo]

Katika nyumba nyingi za kisasa kuna choo cha maji. Hiki mara nyingi ni bakuli ya kauri inayounganishwa na bomba la majichafu na bomba la maji safi la kusukuma kinyesi hadi bombani. Kuna pia mabakuli ya feleji. Kiasi cha maji kinachobaki muda wote kwenye bomba la "S" linazuia kuenea kwa haruu mbaya kutoka mfereji wa majichafu. Wakati wa kumwaga maji yaliyomo yote ya choo kinaingia katika bomba la majichafu na kutoka hapa ama katika tangi ya nyumba au hadi mfumo wa kukusanya majichafu ya kieneo.

Vyoo vya maji vinapatikana ama kama choo cha kukalia ("western toilet") au choo cha kuchuchumaa (zinazojulikana Ulaya kama "choo cha kifaransa" au penginepo mara nyingi kama "choo cha Kiasia").

Tatizo la vyoo vya maji ni matumizi ya maji mengi. Kila safari ya kumwaga lita 9 - 12 zinaweza kupita chooni katika choo cha kawaida. Hapo kuna majaribio mbalimbali za kupunguza matumizi ya maji na vyoo vya kisasa huwa na tangi ambako mtumiaji anaweza kuchagua kama anamwaga kiasi kikubwa au kiasi kidogo. Katika nchi kadhaa kuna mabomba tofauti kwa maji safi ya kunywa na maji kwa matumizi ya choo ambayo hayakusafishwa vile; kuna pia mifumo ya kukusanya maji ya mvua au hata maji yaliyowahi kutumiwa kwa ajili ya mashine ya kuosha nguo au bafuni kwa matumizi ya chooni.

Choo cha maji kwenye meli hutumia maji ya chumvi.

Vyoo vya kemia

[hariri | hariri chanzo]

Kwenye eropleni, kwenye treni za kisasa na pia kwenye magari ya camping kinyesi kinaingia katika tangi yenye kemikali ya majimaji zinazoua bakteria na kutunza akiba ya kinyesi hadi nafasi ijayo ya kumwaga yaliyomo yake. Choo cha aina hii kwenye eropleni au treni kinatumia nguvu ya ombwe yaani sehemu ya tangi huwa na shinikizo chini ya shinikizo la hewa na wakati wa kufungua valvu ya tangi yaliyomo ya bakuli husukumwa ndani na hewa inayoingia kwa kusawazisha shinikizo. Mara baadaye pampu inatoa hewa kwenye tangi kwa kusudi la kurudisha shinikizo la duni.

Lakini vyoo vya kemia kwa ajuili ya magari ya camping na pia vyoo katika kontena ya choo jinsi zinavyowekwa mahali kwa muda tu zinafanana zaidi na choo cha shimo maana kinyesi kinaanguka moja kwa moja katika kemikali ya tangi.

Choo cha shimo

[hariri | hariri chanzo]
Choo cha shimo hatari (Kenya, mwaka 2009)
Choo cha shimo msituni huko Ujerumani, mnamo mwaka 2004

Choo cha shimo ni mfumo unaotumiwa na watu wengi kidogo hasa nje ya miji na pia katika mitaa ya vibanda. Shimo lachimbwa katika ardhi na kufunikwa juu isipokuwa kuacha nafasi ya kuangusha kinyesi. Kwa kawaida kuna nyumba ndogo au kibanda juu yake cha kuzuia watazamaji. Kinyesi kinaanguka katika shimo na kubaki pale. Shimo linajaa polepole lakini kama udongo unafaa majimaji yake hunapotea ardhini ni mambo makavu pekee yanabaki. Lakini penye maji mengi katika ardhi au kama ardhi ina tabia kukaribia udongo wa mfinyanzi maji hayapotei na shimo linajaa haraka.

Kama shimo limejaa inawezekana kuifunika kwa ardhi tu na kuicha jinsi ilivyo lakini mtindo huu unawezekana pale ambako nafasi ya inatosha kuchimba mashimo mapya. Menginevyo kuna njia ya kuondoa uchafu kwenye shimo ka kuipeleka mahali pengine. Katika nchi mbalimbali yaliyomo hutumiwa kama samadi kwenye mashamba hata kama hii inaweza kuwa na hatari kama kinyesi cha juu bado kina bakteria ya kuambukiza au mayai ya minyoo yanayoweza kuambukiza watu wanaolima mashamba husika na kula mavuno yake.

Kuna matatizo ya choo cha shimo na haya ni pamoja na

  • harufu mbaya hasa katika mazingira ya joto
  • hatari ya mafuriko wakati wa mvua mkali ambako yaliyomo ya shimo yanaweza kusambazwa nje
  • machafuko ya akiba ya maji chini ya ardhi kwa mfano visima vilivyo karibu
  • ujenzi mdhaifu unaoweza kusababisha kwa ukuta wa shimo na ajali ya kuanguka mle
  • hatari za afya wakati wa kuondoa yaliyomo ya mashimo

Choo cha samadi

[hariri | hariri chanzo]

Kuna mbinu mbalimbali za kutumia kinyesi cha kibinadamu kama samadi na mbolea katika kilimo. Kimsingi mawi ya kibinadamu sawa na mawi ya wanyama bado ina sehemu ndani yake zinazofaa kama virutubishi vya mimea. Tatizo la kimsingi ni ya kwamba katika kinyesi kibichi kuna hatari ya kuwepo kwa bakteria na vimelea hai kutoka utumbo wa watu wagonjwa hivyo hatari ya kuambukizwa. Hatari hii inakwisha kama kinyesi kinakaa kwa muda wa kutosha na hasa kisipoguswa kwa mkono au sehemu nyingine ya mwili wa kibinadamu.

Kati ya mbinu hizi ni

  • kukusanya kinyesi kwenye shimo pamoja na mata ogania inayoharakisha kuoza chake hadi kuwa udongo mwenye rutba. Majani makavu na ganda la miti lililosagwa au unga wa ubao vinafaa kwa kazi hii. Kikemia kinyesi huwa na nitrojeni nyingi na kukichanganya na mata yenye kaboni nyingi kunasaidia kukiingiza katika mchakato wa kikemia kwa haraka. Shimo lisilo ndefu linafunikwa kwa ganda la mata ogania na baada ya kila matumizi ya choo mata hii inamwagikwa tena kuu ya kinesi kipya. Harufu mbaya hupunguka sana kulingana na mashimo ya kawaida, majimaji hunyonywa na majani au unga wa ubao na bakteria za kuozesha yote yana mazingira ya kufaa. Yaliyomo yanaweza kutolewa kirahisi zaidi kwa sababu shimo si ndefu sana na baada ya miezi kadhaa ya kukaa bakteria hatari na vimelea vimekufa. Sasa ule unaonekana kama udongo na usio na harufu tena unaweza kuchimbwa katika matuta ya bustani au kwenye shamba. Mtindo huu haufai kwa matumizi ya watu wengi.
  • njia iliyotumiwa tangua miaka kadhaa ni kuchimba mashimo madogo zaidi kama choo cha kawaida halafu kupanda miti kando la shimo, hasa miti inayokua haraka, pia miti ya matunda na ndizi. Baada ya shimo kujaa miti au ndizi inaweza kupandwa juu ya mahali pa shimo ambalo sasa limekuwa mahali pa rutba[4] [5] [6].

Choo cha kugandisha

[hariri | hariri chanzo]

Huko Skandinavia watu wamebuni choo ambako kinyesi kinagandishwa kwa baridi [7].

Choo hiki kilibuniwa huko Uswidi na siku hizi hutengenezwa nchini Finland. Kinatumia umeme kikifanya kazi kama friji. Kinyesi kinagandishwa na hivyo bakteria haziwezi kuendlea hakuna harufu mbaya. [8][9] Hakuna haja ya maji au kemikali.[10]

  1. Curtis V, Aunger R, Rabie T: Evidence that disgust evolved to protect from risk of disease, Proc. Biol. Sci. Vol 271 Suppl 4 , uk. 131–3 May 2004
  2. Kumb. 23,12
  3. "Progress on Sanitation and Drinking Water: 2015 Update and MDG Assessment" (PDF). 2015. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2016-03-04. Iliwekwa mnamo 1 Oktoba 2015.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. Tree bog kwenye tovuti ya pemacuture - mbinu hii ilianzishwa Uingereza mnamo 1995 na miti iliyotumiwa pale ni hasa aina ya willows
  5. How to build a tree bog composting toilet
  6. Promoting human compostig in Haiti
  7. "Google Translate". google.com. Iliwekwa mnamo 16 Mei 2015.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  8. Mario Aguilar. "Toilet Freezes Your Poop To Keep It From Stinking". Gizmodo. Gawker Media. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2016-03-04. Iliwekwa mnamo 16 Mei 2015.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  9. "Literature - Käymäläseura Huussi". huussi.net. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-09-24. Iliwekwa mnamo 2015-11-21.
  10. "Full papers - Käymäläseura Huussi". huussi.net. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-09-24. Iliwekwa mnamo 2015-11-21.

Kujisomea

[hariri | hariri chanzo]