Hijabu

Wanawake wa Kiislamu ndani ya vazi la hijabu huko Brunei.

Hijabu (kutoka Kiarabu: حجاب hijab) ni kitambaa au vazi linalovaliwa na wanawake, hasa wa Kiislamu, mbele ya mwanamume yeyote nje ya familia yao. Vazi hilo kwa kawaida hufunika kichwa na kifua. Neno hilo linaweza kumaanisha vazi lolote lenye kufunika kichwa, uso, au mwili mzima kinachovaliwa na wanawake wa Kiislamu kinacholingana na viwango vya Kiislamu vya staha.

Kawaida yake inaweza kuwa tofauti kati ya madhehebu ya Waislamu na nchi. Mara nyingi inataja tu kitambaa kinachofunika nywele; kuna mitindo unaofunika sehemu za mwili pia au mwili wote pamoja na uso na mikono.

  • Buibui ni hijabu ya kimapokeo ya wanawake Waswahili, ni vazi jeusi likifunika kichwa na mwili
  • Chador ni hijabu ya Iran ikivaliwa pia kati ya Washia Ithnashari Waarabu; ni kipande kimoja cha kitambaa kinachowekwa juu ya kichwa na kufungwa mbele kwa mkono mmoja. Inaweza kuwa na rangi na picha za maua, lakini tangu mapinduzi ya Kiislamu ya Iran inatumiwa mara nyingi kwa rangi nyeusi tu
  • Burka ni hijabu hasa ya Afghanistan; ni vazi lenye umbo la gunia lenye nafasi ya nyavu mbele ya uso inayoruhusu kuangalia nje
  • Nikabu ni hijabu inayofunika kichwa na mabega pamoja na uso, ikiacha nafasi tu kwa macho

Hijabu ya Kiislamu

[hariri | hariri chanzo]

Kwa ujumla, katika Uislamu, hijabu ni vazi la kisheria linalositiri mwili wote wa mwanamke isipokuwa uso na vitanga vya mikono, vazi ambalo halionyeshi umbo la mvaaji au mikatiko ya mwili wake. Vazi hilo ni faradhi kwa kila mwanamke wa Kiislamu kwa amri iliyowekwa na Mwenyezi Mungu ili kulinda hadhi ya mwanamke. Hivyo WaislamU wote, bila kujali madhehebu zao, wanalazimika kutii amri hiyo: “Haiwi kwa muumini mwanaume wala muumini mwanamke, Mwenyezi Mungu na mtume wake wanapoamua jambo kua na khiyari katika jambo hilo, na yeyote mwenye kumuasi mwenyezimungu na mtume wake amepotea upotovu ulio wazi”. (33:36)

Ni wajibu kuufahamisha ulimwengu mzima ya kwamba mwanamke ni kiungo muhimu katika jamii, na anayo haki na heshima kama mtu mwingine yeyote anayeishi katika dunia. Kwa kuWa Uislamu ni dini inayoshughulikia kila uwanja wa maisha ya mwanadamu, imetoa umuhimu pekee katika kulinda na kutetea utu, heshima pamoja na haki za mwanamke, hivyo basi Uislamu umemuekea kanuni za sharia zitakazomfaa kulingana na mazingira yake, iwe maisha ya peke yake, ndani ya ndoa, familia na jamii kwa ujumla. Maumbile ya mwanamke yanapoangaliwa kwa umakini hapana shaka yoyote kuwa yanatofautiana na maumbile ya mwanamume kisaikolojia na katika mazingira fulani ya kijamii.

Ndani ya Qur’an zipo aya nyingi zinazozungumzia miongozo mbalimbali juu ya mwanamke, ikiwemo namna ya mienendo na mavazi yake na haki zake ndani ya jamii, hivyo hijabu ndiyo alama pekee ya kumtambulisha mwanamke mwenye kujiheshimu. Kama ambavyo Allah anavyosema katika Qur’an yake: “Ewe nabii, waambie wake zako na mabinti zako na wanawake waaminio, wateremshe shungi zao kwa kufanya hivyo kutapelekea wao kutambulikana (kwamba ni wanawake waungwana, hawatakerwa na watu waovu), na Allah ni mwingi wa kusamehe tena ni mwingi wa huruma”. Qur'an 33:89

Katika aya hii Mwenyezi Mungu anamuamuru nabii wake Muhammad awaamrishe wanawake wa Kiislamu wakiwemo wake zake na mabinti zake na wanawake waaminio kwa kujisitiri na kuvaa hijabu iliyokamilika kisheria. Katika zama za mwanzo za Uislamu, wanawake walikuwa wakitoka nyumbani mwao bila kujisitiri miili yao kikamilifu kama vile walivyokuwa wakitoka wanawake wa zama za kijahilia (kabla ya uislamu), hali ya kutojisitiri kwa wanawake haikuridhiwa kwa sharia za Kiislamu. Ndipo Mwenyezi Mungu alipomuamuru mtume wake awaambie wanawake wake waumini wajisitiri na wavae hijabu na awakataze wasitoke nyumbani bila ya sitara iliyokamilika kuisheria.

Ama maana inayopatikana kwa kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema kufanya hivyo kutapelekea wao kueleweka (kwamba wao ni wanawake waungwana) kauli hii inalenga kufahamisha kuwa hijabu humfanya mwanamke atajwe kwa utajo wa wema katika jamii, na hupambika kwa sifa ya uchamungu. Mungu anasema kumwambia nabii wake: “Na kaeni majumbani mwenu (enyi wanawake) na wala msionyeshe mapambo yenu kama walivyokua wakionyesha mapambo yao wanawake wa zama za jahilia (kabla ya kuja uislamu)”.

Aya hii inamtaka mwanamke asionyeshe mapambo yake kwa wanaume wengine na watulie nyumbani mwao ili tu wao sio watu wa kazi za nje. Akasema Allah: “Na mnapowauliza kitu wake za mtume waulizeni nyuma ya pazia kufanya hivyo kutatakasa nyoyo zenu na nyoyo zao”. Maana ya aya hii ni kupatikana wajibu wa kuwepo sitara yaani, hijabu baina ya wanaume na wanawake, sio sawa waume na wake kukosa mipaka ya mawasiliano.

Aliposema Mwenyezi Mungu kufanya hivyo kutatakasa nyoyo zenu na nyoyo zao, kilichokusudiwa ni suala la hijabu, kwa maana halisi ni jambo jema kwa pande zote mbili, wanaume na wanawake. “Enyi wanadamu hakika tumewateremshia vazi lifichalo aibu (Tupu) zenu na vazi la pambo, na vazi la taqwa ndilo bora. Hiyo ni katika ishara ya mwenyezimungu ili wapate kukumbuka”. (Qur'an 7;26)

Sifa za hijabu ya Kiislamu

[hariri | hariri chanzo]

1. Kitambaa kiwe kizito 2. Kitambaa kisiwe na mapambo (urembo) 3. Isiwe ni nguo yenye kubana

Hijabu ni lazima ifunike mwili wote wa mwanamke. Hadithi za mtume zinaelezea pia jinsi mwanamke wa Kiislamu anavyotakiwa kujisItiri kwa mujibu wa sharia za Kiislamu. Haifai kuonyesha sehemu za mwili, hivyo mwanamke ajisItiri maungo yake sawasawa. Amesema mtume, “Ni haramu kwa mwanamke muumini, aliyemuamini Mwenyezi Mungu na mtume wake na siku ya mwisho kuacha wazi mikono yake wazi zaidi ya kitanga cha mkono" (imepokewa na ibn Jaabir).

Aina ya kitambaa

[hariri | hariri chanzo]

Nguo aivaayo mwanamke wa Kiislamu, lazima iwe nzito, isiwe nyepesi kiasi cha kuonyesha rangi ya ngozi ya mwili wa mvaaji.

Nguo isiwe na mapambo

[hariri | hariri chanzo]

Hijabu inayofaa huwa haina mapambo yoyote ya kung’aa na kuifanya iwe ni yenye kuvutia machoni mwa watu hasa wanaume na kusababishwa kutamaniwa.

Nguo kutoashiria ukafiri
[hariri | hariri chanzo]

Nguo aivaayo mwanamke wa Kiislamu kwa ajili ya sitara isivaliwe kwa nia ya ria (kujionyesha) kiburi au fahari. Mtume Muhammad ametuachia usia wa namna hiyo: “Yule ambaye atavaa mavazi yake kwa ajili ya ufakhali katika dunia, Allah (s.w.t) atamvisha mavazi ya izara siku ya malipo na atayatumbukiza motoni mavazi hayo.” Akasema tena, “Mwenye kiburi hata chembe moja ya mchele hataingia peponi”. Mtume amesema: “Katika zama za mwisho watakuja watu katika umma wangu ambao wanawake zao watavaa nusu na nusu watakua uchi. Vichwani watasuka mafundo ya nywele na kuyaacha wazi bila ya kujifunika. Basi sikilizeni niwaambieni, kuweni ni wenye kuwalaani wanawake hawa kwani tayari wamekwisha laaniwa, wala hawatapata harufu ya pepo kwani ipo mbali nao kwa mwendo wa miaka mia tano”.

Imepokewa kutoka kwa Imamu Ally akisema, “katika zama za mwisho kitakapokua kiama kinakaribia, watatoka wanawake watakaokuwa uchi, bila ya kujistiri miili yao kisheria, wanawake hawa watakuwa wametoka katika dini na wataingia katika fitina, watapenda starehe na mambo ya fahari na watahalalisha mambo haramu na kuharamisha mambo halali. Wanawake hawa malipo yake ni kuingia motoni. Basi angalieni sana, kipindi hicho ni kibya sana kuliko vipindi vingine”.

Upana wa nguo

[hariri | hariri chanzo]

Nguo atakiwayo kuivaa mwanamke wa Kiislamu isiwe ya kubana, iwe pana ya kutosha ili asionyeshe umbile lake.

"Kujiheshimu" ndio pambo la mwanamke

[hariri | hariri chanzo]

Mtume amesema, “Kujiheshimu ndio pambo la mwanamke”. Pambo limegawanyika katika sehemu mbili: a) Pambo halisi b) Pambo lisilo halisi

Pambo halisi

[hariri | hariri chanzo]

Pambo hili ni lenye kubaki muda wote, pia humfanya mwanamke apate ule utukufu wake kamili na kumfikisha kwenye daraja la ukamilifu.

Pambo lisilo halisi

[hariri | hariri chanzo]

Ama pambo lisilo halisi ni lile ambalo linaonekana wazi na ni lenye kubaki kwa muda maalumu kisha hutoweka bila ya kumuongezea kitu mhusika katika utu wake.

Ukweli usio na shaka ni kua pambo halisi ni lenye umuhimu mno kuliko pambo lisilo halisi,na ndio lengo linalopaswa kushikiliwa na kila mtu. Endapo mtu atakosa kuwa na fungamano fulani katika pambo hilo halisi basi pia hua hana faida na pambo lisilo halisi (pambo la dhahiri).

Hapana shaka "kujiheshimu" ndio pambo pekee kama alivyosema mtume wa m/mungu kwamba pambo hilo humjengea mwanamke utu wake,heshima yake na utukufu hapa duniani na kesho akhera. Ama madawa ya kujirembesha, manukato na mengineyo miongoni mwa mapambo yoyoye hayo ni mapambo ya nje tu na hayana maana yoyote hususan atakapokua mwanamke mwenyewe si mchamungu.

Hijabu ndio vazi pekee litakalomtambulisha mcha Mungu mwanamke, utu wake na heshima yake. Tabia ya kutovaa hijabu huufanya mwili wa mwanamke kuwa sehemu ya maonyesho kwa maelfu ya watu siku zote.

Imam Ally amesema “yeyote mwenye kuiweka nafsi yake mahali penye tuhuma mbaya basi asimlaumu mtu atayemdhania vibaya”. Hapana shaka mwanamke asiyekua na hijabu hua anadhurumu nafsi yake mwenyewekwa; sababu, kwanza huwa anapata hasara mbele ya mwenyezimungu na pili heshima yake ndani ya jamii inaporomoka.

Kwa hasara anayoipata mbele ya mungu ni kua amekwenda kinyume na kanuni na maamrisho ya m/mungu kwa kukosa utii kwa muumba wake.

Ama hasara anayoipata kutokana na kuporomoka kwa heshima yake ndani ya jamii kutokana na tabia yake ya kuacha mwili wake wazi ili aonekane na kila mtu, hali hiyo humuingiza katika kila aina ya uovu na ufisadi na hatimaye kudhalilika vibaya.

Ama mwanamke mwenye kujisitiri vizuri kwa mujibu wa sharia za Kiislam hupata faida za aina mbili, faida aipatayo mbele ya Mwenyezi Mungu, yeye huwa mwanamke mtukufu mbele ya Mwenyezi Mungu pamoja na malaika wake na mawalii wa Mungu, utukufu huu anapata kwa kuwa amemtii Mwenyezi Mungu aliye mtukufu ambaye ni Mola wa viumbe wote. Vilevile kwa kuwa ametekeleza maamrisho yake kwa kujisitiri maungo yake ambayo Mwenyezi Mungu ameamrisha yasitiriwe, basi kila anyanyuapo unyayo wake rehema za Mwenyezi Mungu huwa zipo pamoja naye pamoja na radhi zake, na wakati huohuo malaika wa Mwenyezi Mungu humuombea msamaha na Mwenyezi Mungu anamsamehe.

“Basi chochote mtachopewa ni starehe ya maisha ya dunia lakini kilichopo kwa mwenyezi mungu ni bora na cha kudumu zaidi kwa ajili ya walioamini na wakawa wanamtegemea mola wao”. (Qur’an, 42:36)

Ama faida inayopatikana katika jamii ni pale mwanamke huyo anapokuwa ni mwenye kuheshimiwa na kutukuzwa. Yote haya yanapatikana kwa kuwa amejipamba kwa pambo la kujiheshimu (uchamungu) na kujihifadhi mwili wake huo aliopewa na Mwenyezi Mungu kwa kuvaa hijabu.


Marejeo mengine

[hariri | hariri chanzo]
  • Ahmed, Leila (1992). Women and Gender in Islam: Historical Roots of a Modern Debate. New Haven: Yale University Press. ISBN 978-0-300-05583-2.
  • Aslan, Reza, No god but God: The Origins, Evolution, and Future of Islam, Random House, 2005
  • Bloom, Jonathan; Blair, Sheila (2002). Islam: A Thousand Years of Faith and Power. Yale University Press. ISBN 978-0-300-09422-0.
  • El Guindi, Fadwa (1999). Veil: Modesty, Privacy, and Resistance. Oxford: Berg. ISBN 978-1-85973-929-7.
  • Elver, Hilal. The Headscarf Controversy: Secularism and Freedom of Religion (Oxford University Press; 2012); 265 pages; Criticizes policies that serve to exclude pious Muslim women from the public sphere in Turkey, France, Germany, and the United States.
  • Esposito, John (2003). The Oxford Dictionary of Islam. Oxford University Press. ISBN 978-0-19-512558-0.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hijabu kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.