Mapinduzi ya Ufaransa

Uhuru (wenye sura ya mwanamke) unaongoza wananchi katika mapinduzi (Mchoro wa Eugène Delacroix).

Mapinduzi ya Ufaransa (kwa Kifaransa: Révolution française) ni jina linalojumlisha matukio muhimu ya siasa kwa kipindi cha miaka 10, tangu 1789 hadi 1799, yaliyobadilisha uso wa Ufaransa na utamaduni wa Ulaya kwa jumla, kiasi cha kuhesabiwa kati ya matukio makuu ya historia yote.[1][2][3]

Kupitia vita mbalimbali vilivyofuata katika sehemu mbalimbali za dunia,[4] athira zake zilieneza kote duniani fikra za haki za binadamu, uhuru na maendeleo zilizotetewa na Falsafa ya Mwangaza.[5]

Dhana ya kuwa mamlaka juu ya dola ni haki ya raia wote, si ya wafalme wala watawala wengine,[6] imeenea polepole pande zote za dunia.[7]

Pamoja na hayo, mapinduzi na matukio yaliyofuatwa yalisambaza mtazamo hasi kuhusu dini, huhusan Ukristo na Kanisa Katoliki, kwa kudai akili ishike nafasi ya imani pia.

Muhtasari wa mapinduzi

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1789 mfalme Louis XVI alilazimishwa kuitisha bunge la taifa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 170. Sababu yake ilikuwa kwa kiasi kikubwa cha madeni ya serikali yaliyosababishwa na matumizi makubwa ya mfalme pamoja na gharama za vita vya uhuru vya Marekani vilivyosaidiwa na Ufaransa dhidi ya Uingereza.[8]

Tangu Louis XIV (16431715) wafalme walitawala Ufaransa bila bunge, lakini kisheria mfalme hakuwa na madaraka ya kuongeza kodi bila idhini ya bunge, na Louis XVII hakuwa tena na nguvu ya kutosha kupuuzia utaratibu huo.

Bunge la Ufaransa lilikuwa na wawakilishi wa matabaka matatu: koo za makabaila, wawakilishi wa Kanisa Katoliki na wawakilishi wa tabaka la tatu yaani raia waliolipa kiasi fulani cha kodi. Maskini na wanawake hawakuwa na wawakilishi.

Wawakilishi wengi wa tabaka la tatu walidai kupewa nafasi kubwa zaidi kuliko matabaka mengine. Baada ya matatizo ya kutoelewana, kwenye tarehe 17 Juni 1789 wawakilishi wa tabaka la tatu walijitangaza kuwa bunge la taifa hata bila ya wawakilishi wa waungwana waliotetea haki zao za kale.

Kutokana na vurugu za kisiasa na mfumuko wa bei za chakula, wananchi wa Paris waliasi, wakashambulia gereza la Bastille tarehe 14 Julai na kulibomoa. Tarehe hiyo hadi leo ni sikukuu ya mapinduzi nchini Ufaransa. Mfalme aliyedhoofika hakutaka kukandamiza uasi huo na bunge la taifa liliendelea kubadilisha sheria kwa kufuta haki za pekee za waungwana. Mashambani wakulima walianza kuasi na kukataa ulipaji kodi katika mikoa mbalimbali.

Mfalme alipoona ya kwamba madaraka yake yanapungua zaidi na zaidi alijaribu kuondoka lakini alikamatwa na kurudishwa kama mfungwa mwaka 1791.

Mwelekeo mkali kati ya wabunge ulipata ushindi na mwaka 1792 Ufaransa ulitangazwa kuwa jamhuri. Mfalme alishtakiwa kuwa msaliti wa taifa akapewa hukumu ya kifo na kukatwa kichwa pamoja na mke wake tarehe 21 Januari 1793.

Wafalme wa nchi jirani waliamua kushambulia Ufaransa na kulipiza kisasi kwa kifo cha mfalme. Katika joto la vita watu wa vikundi vikali vilipata kipaumbele wakaanzisha kipindi cha udikteta chini ya kamati ya bunge lililoongozwa na Robespierre. Watu wengi (16,000-40,000) walishtakiwa kuwa wasaliti wakauawa[9] hadi upinzani ndani ya bunge ulipofaulu kuwakataa viongozi wakali na kuwaua.

Kipindi kilichofuata kilikuwa na serikali zilizochaguliwa na bunge. Zililenga kurudisha utaratibu nchini na kutetea taifa katika vita vilivyoendelea hasa dhidi ya Uingereza na Austria.

Katika vita hivyo jenerali Napoleon Bonaparte alikuwa kiongozi aliyeweza kushinda Austria akawa shujaa wa taifa. Mwaka 1799 kwa tishio la kijeshi alilazimisha bunge kubadilisha katiba akaingia serikalini na kuwa mtawala pekee kwa kibali cha bunge lisilokuwa na njia nyingine isipokuwa kumkubali.

Tangu hapo Napoleon alitawala kwa cheo cha "konsuli wa kwanza". Baada ya mabadiliko mengine ya katiba alichukua cheo cha Kaisari wa Ufaransa mwaka 1804.

Sababu za mapinduzi

[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya mapinduzi Ufaransa ulitawaliwa na wafalme. Mfalme Louis XIV aliwahi kuunganisha mamlaka yote ya dola mikononi mwake akifaulu kukandamiza upinzani wote wa waungwana na malodi. Utawala huo wenye madaraka yote uliendelea chini ya waaandamizi wake. Kila azimio lilitegemea mapenzi ya mfalme bila njia yoyote ya upinzani.

Ufaransa haukuwa na bunge la kudumu; palikuwa na mabunge ya kimkoa ambako wawakilishi wa waungwana na makasisi wakuu wa Kanisa Katoliki (iliyokuwa dini pekee halali kisheria) walikutana, wakati mwingine pamoja na wawakilishi kadhaa wa tabaka la tatu lililojumlisha watu wengine wote wenye mali. Bunge la taifa lililokuwa na madaraka ya kuamua juu ya sheria za kodi hasa liliwahi kualikwa mara kadhaa na wafalme lakini tangu Louis XIV halikukutana tena.

Mwaka 1789 utawala huo ulishikwa na mchafuko. Wafalme waliwahi kutumia pesa vibaya na nchi ilikuwa na madeni makubwa. Madeni hayo yalisababishwa na vita, matumizi makubwa kwa maafisa wa serikali na gharama za familia ya kifalme, kwa mfano ujenzi wa majumba ya kifalme na sherehe za mfalme.

Katika jamii ya Ufaransa vikundi viwili vilikuwa na haki nyingi, yaani familia za waungwana na makasisi wa Kanisa Katoliki. Hao hawakulipa kodi ingawa walikuwa na mashamba makubwa yaliyolimwa na wakulima waliopaswa kuwalipia mchango wa mavuno. Kodi zote za nchi zililipwa na wakulima au wafanyabiashara wa mjini.

Mwaka 1788 ulikuwa na mavuno mabaya na wakulima wengi hawakujua jinsi ya kulipa kodi zao. Ghala za waungwana na za makanisa zilijaa kutokana na mavuno ya miaka ya nyuma, lakini kwa jumla bei ya nafaka ilipanda pamoja na bei ya mkate uliokuwa chakula kikuu cha Wafaransa.

Viongozi wa serikali chini ya mfalme waliona haja ya mabadiliko lakini matabaka tawala ya waungwana na viongozi wa Kanisa hawakuwa tayari kukubali mabadiliko yoyote.

Bunge la matabaka matatu

[hariri | hariri chanzo]

Mnamo Februari 1789 serikali ilialika mkutano wa wawakilishi wa waungwana na makasisi wakuu ikatafuta kibali chao kwa sheria mpya, eti hata waungwana walipe kodi. Mkutano ulikataa ukidai hauna madaraka ya kubadilisha sheria za kale, lakini ilikuwa wazi kwamba hiyo ilikuwa lugha tu ya kuepukana na kodi.

Hivyo serikali ilimshauri mfalme kualika bunge la kitaifa la matabaka yote matatu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1614. Zamani bunge hilo lilikuwa na idadi sawa ya wawakilishi kwa kila tabaka yaani 300-300-300 kwa waungwana, makasisi na tabaka la tatu. Tena kila tabaka lilikuwa na kura moja tu, kwa hiyo kila azimio lilihitaji kura zote tatu au kura mbili dhidi ya moja.

Kabla ya mkutano huo wawakilishi wa tabaka la tatu walidai kuongezeka kwa kura zao wakieleza ya kwamba hadi sasa tabaka lao lililipa kodi zote na kuwakilisha zaidi ya asilimia 90 za wananchi. Mfalme alihangaika akakubali tabaka la tatu liwe na wawakilishi 600, isipokuwa alikaa kimya juu ya suala la kura.

Uvamizi wa Bastille tarehe 14 Julai 1789.

Kujitenga kwa tabaka la tatu kuwa bunge la taifa

[hariri | hariri chanzo]

Bunge lilikaa wiki kadhaa bila ya makubaliano juu ya namna ya kupiga kura. Baada ya mwezi mmoja sehemu ya mapadri walijiunga na wawakilishi wa tabaka la tatu kutetea azimio lililopelekwa na kasisi Abbe Siyes: tabaka la tatu likajitangaza kuwa linawakilisha asilimia 96 za wananchi likajiita "bunge la taifa". Wawakilishi wa waungwana na makasisi wengine walialikwa kujiunga nao kwenye msingi wa kura moja kwa kila mbunge.

Makasisi wengi na waungwana wachache walifuata wito huo, lakini kundi kubwa la waungwana walikataa wakadai mfalme aingilie kati. Mfalme Louis XVI alitangaza mkutano mpya chini ya utaratibu wa kale akafunga ukumbi wa mkutano hadi siku hiyo.

Wawakilishi wa bunge la taifa waliamua kukutana mahali penginepo wakaahidiana kutoachana hadi katiba ya taifa itakapokuwa tayari. Mfalme aliamuru waondoke lakini mwenyekiti wao alikataa. Mfalme aliandaa vikosi vya jeshi lakini sehemu za waungwana walimwomba asitumie silaha. Mwishowe mfalme alikata tamaa akaamuru matabaka yote yakae pamoja katika bunge la taifa.

  1. Linda S. Frey and Marsha L. Frey, The French Revolution (2004), Foreword.
  2. R.R. Palmer and Joel Colton, A History of the Modern World (5th ed. 1978), p. 341
  3. Ferenc Fehér, The French Revolution and the Birth of Modernity, (1990) pp. 117-30
  4. Bell, David Avrom (2007). The First Total War: Napoleon's Europe and the birth of warfare as we know it. New York: Houghton Mifflin Harcourt. uk. 51. ISBN 0-618-34965-0.
  5. Suzanne Desan et al. eds. The French Revolution in Global Perspective (2013) , pp. 3, 8, 10
  6. Livesey, James. Making Democracy in the French Revolution p. 19 The Revolution created and elaborated...the ideal of democracy, which forms the creative tension with the notion of sovereignty that informs the functioning of modern democratic liberal states. This was the truly original contribution of the Revolution to modern political culture.
  7. Palmer, R.R. & Colton, Joel A History of the Modern World p. 361
  8. Tombs, Robert and Isabelle. That Sweet Enemy: The French and the British from the Sun King to the Present. Random House (2007) ISBN 978-1-4000-4024-7. Page 179.
  9. Matusitz, Jonathan Symbolism in Terrorism: Motivation, Communication, and Behavior, p. 19

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mapinduzi ya Ufaransa kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.