Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokea tarehe 26 Aprili 1964 ukawa mwanzo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hadi tarehe ile kulikuwa na mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa dola la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.[1]
Mkataba wa Muungano
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar. Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi tarehe 26 Aprili 1964[2].
Tarehe 27 Aprili 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano.[3]
Mabadiliko ya jina
Jina la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa baadaye, tarehe 28 Oktoba 1964, na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.[4]
Muundo wa Muungano
Muundo wa Muungano wa Tanzania kama ulivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, una vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Zanzibar; na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashughulikia mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Visiwani.[5]
Sababu ya Muungano
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu mbalimbali kama vile kuwepo kwa mahusiano ya karibu na ya kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile undugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususan baina ya vyama vya TANU na ASP.
Pia, azma ya kuwa na Muungano wa Afrika, hususan kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki. Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania uhuru katika ukanda wa Afrika walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika. Mwalimu Nyerere binafsi alipendelea uwepo Muungano wa Afrika kwa kuanzia na Mashirikisho ya kikanda.
Kimsingi zipo sababu mbalimbali zilizosababisha Muungano huu kama vile historia za nchi hizo mbili, ukaribu wa nchi hizi mbili, muingiliano wa kijamii, ushirikiano wa kibiashara, ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu wa kisiasa baina ya TANU na ASP, ushirikiano na urafiki wa muda mrefu kati ya watu, viongozi, na wakati wa harakati za utaifa uliopelekea uhuru wa nchi hizo mbili.[6]
Hati za makubaliano ya muungano
Msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati za Muungano za mwaka 1964. Hati za Muungano zilitiwa saini na waasisi wa Muungano tarehe 22 Aprili 1964, na kupelekea Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Baada ya Muungano, Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya ya Muungano wa Tanzania na Sheikh Abeid Amani Karume, alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aprili 26, 1964 Bunge la Tanganyika lilipitisha Sheria za Muungano. Halikadhalika, Sheria hizo zilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar. Sheria hizo za Muungano zilithibitisha Hati za Muungano, zilitaja Rais na Makamu wa Rais, zilitaja Muundo wa Muungano na Katiba ya Muungano.[7]
Mabadilishano za hati baina za waasisi
Aidha, Aprili 27, 1964, waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za Muungano na wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Sheikh Abeid Amani Karume, Kassim Abdala Hanga, Abdulrahaman Mohamed Babu, Hassan Nassor Moyo, Sheikh Aboud Jumbe, Hasnu Makame na Sheikh Idris Abdul Wakil. Baada ya kuapishwa kuwa wabunge wakateuliwa kuwa mawaziri wa Serikali ya Muungano.
Kabla ya muungano
Kabla ya Muungano, kulikuwa na Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1962 na upande wa Zanzibar kulikuwa na Amri za Katiba (Decrees). Katiba ya Tanganyika baada ya kufanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya Muungano iliendelea kutumika kama Katiba ya Muungano ya mpito hadi mwaka 1977 ilipopitishwa Katiba ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria za Muungano.
Aidha, marekebisho hayo yalimtaja Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwa msaidizi wa Rais kwa masuala yote ya kiutawala kwa upande wa Zanzibar, na Waziri Mkuu kuwa ni Makamu wa Pili wa Rais ambaye atamsaidia Rais kwa masuala yahusuyo upande wa Tanganyika na kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni.
Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliainisha mambo kumi na moja ambayo yalikubalika kuwa ni ya Muungano chini ya usimamizi wa Serikali ya Muungano ambayo ni pamoja na Katiba na Serikali ya Muungano. Mambo hayo ni: Mambo ya Nchi za Nje; Ulinzi; Polisi; Mamlaka juu ya mambo yanohusika na hali ya hatari; Uraia; Uhamiaji; Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje na Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Mambo mengine ni Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha; na Bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu.[8]
Kuongezeka kwa orodha ya mambo ya muungano
Mambo ya Muungano yaliongezwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kwa kushirikisha pande zote mbili za Muungano. Juni 10, 1965, mambo yote yahusuyo sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yoyote halali (pamoja na noti); benki (pamoja na zile za kuweka akiba) na shughuli zote za kibenki; fedha za kigeni na usimamizi wa mambo yanayohusu fedha za kigeni yaliingizwa kuwa jambo la 12 la Muungano.
Lengo kubwa la kuongezwa kwa jambo hilo lilikuwa kuwa na sarafu ya pamoja ya Tanzania baada ya Muungano, na kurahisisha usimamizi wa fedha za kigeni na benki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwaka 1964.[9]
Baada ya kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki 1964
Baada ya kuvunjika kwa Bodi hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu na mipango yake ya kusimamia mambo ya kibenki na fedha. Kufuatia kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967, tarehe 11 Agosti 1967 mambo mawili yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano ambayo ni leseni za viwanda na takwimu (Jambo la 13), na elimu ya juu (Jambo la 14).
Mwaka 1968, suala la maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia liliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano kuwa Jambo la 15. [10]
Kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Vilevile, kufuatia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 na kutungwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, mambo yafuatayo yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano ambayo ni Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania na mambo yanayohusika na kazi za Baraza hilo (Jambo la 16); Usafiri; Usafirishaji wa Anga (Jambo la 17) na Utafiti (Jambo la 18); Utabiri wa Hali ya Hewa (Jambo la 19); na Takwimu (Jambo la 20).
Kutokana na kuvunjika kwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki mwaka 1979, suala la Mahakama ya Rufani ya Tanzania nalo liliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa Jambo la 21. Vilevile, kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Nyalali iliyokusanya maoni ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, Uandikishaji wa Vyama vya Siasa na mambo mengine yanayohusiana nayo, liliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano (Jambo la 22). Suala hilo hatimaye lilipitishwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura Namba 258.
Utaratibu uliotumika katika kuongeza idadi ya Mambo ya Muungano kutoka 11 hadi kufikia 22 ni kupitia maamuzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. [11]
Hitimisho
Muungano umechukua nafasi kubwa katika kuwaunganisha wananchi na kuimarisha mahusiano mazuri baina ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wigo mpana kwa wananchi wake kuweza kuzitumia fursa mbalimbali zilizopo za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa lengo la kujipatia maendeleo. [12]
Viungo vya nje
- Historia ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Tanzania) - YouTube
- Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar - Dodoma
Tanbihi
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ https://www.mwananchi.co.tz/mw/habari/kitaifa/muungano-uligubikwa-na-siri-hofu--3797086
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.
- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-09-22. Iliwekwa mnamo 2020-05-30.