Polycarp Pengo

Polycarp Pengo.

Polycarp Pengo ni kardinali wa pili kutoka Tanzania, akiwa aliteuliwa mara baada ya kifo cha Laurean Rugambwa, kardinali wa kwanza kutoka kusini kwa Sahara.

Alizaliwa Mwazye (Wilaya ya Kalambo, mkoa wa Rukwa) tarehe 5 Agosti 1944.

Baada ya masomo ya ngazi mbalimbali, alipewa upadrisho mwaka 1971 na askofu Charles Msakila wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, akasoma teolojia ya maadili huko Roma, Italia, akijitwalia digrii ya udaktari mwaka 1977.

Kisha kufundisha somo hilo kwa muda mfupi kwenye seminari kuu ya Kipalapala (mkoa wa Tabora), alichaguliwa kuwa gombera wa seminari kuu ya Segerea hadi mwaka 1983.

Aliteuliwa askofu wa Nachingwea tarehe 11 Novemba 1983, akapewa daraja takatifu hiyo na Papa Yohane Paulo II tarehe 6 Januari 1984.

Tarehe 17 Oktoba 1986 alihamishiwa jimbo jipya la Tunduru-Masasi.

Tarehe 22 Januari 1990 alifanywa askofu mwandamizi wa Dar-es-Salaam na mwaka 1992, kardinali Laurean Rugambwa alipostaafu, akawa askofu mkuu.

Aliteuliwa na Yohane Paulo II kuwa kardinali tarehe 21 Februari 1998, akikabidhiwa parokia ya Nostra Signora de La Salette mjini Roma.

Pamoja na majukumu mbalimbali katika idara za Papa, tangu mwaka 2007 hadi 2013 alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Afrika na Madagaska.

Tarehe 15 Agosti 2019 ombi lake la kustaafu kama askofu mkuu wa Dar es Saalam lilikubaliwa na Papa Fransisko.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]