Teresa wa Yesu

Mt. Teresa alivyochorwa na Pieter Paul Rubens
Mt. Teresa alivyochorwa na Pieter Paul Rubens
Livio Mehus, Mtakatifu Petro wa Alkantara akimkomunisha mtakatifu Teresa wa Avila; picha ya mwaka (1683) inayotunzwa Prato (Italia)
Teresa nje ya nafsi yake alivyochongwa na Gianlorenzo Bernini katika marumaru, basilika la Santa Maria della Vittoria, Roma.

Teresa wa Yesu (Avila, Hispania, 28 Machi 1515 - Alba de Tormes, Hispania, usiku wa kuamkia tarehe 15 Oktoba 1582) ni jina la kitawa la Teresa Sánchez de Cepeda Ávila y Ahumada, maarufu pia kama Teresa wa Avila.

Mwanamke halisi, bikira, utu wake ulikomaa: alikuwa na tabia ya kupendeza, uchangamfu na busara sana, uhodari na msimamo, uwezo wa kukubali hali iliyopo kwa kupanga vizuri na kufanikisha mambo.

Kisha kujiunga na monasteri ya Wakarmeli, akawa mama na mwalimu wa urekebisho kamili wa shirika lake, akikakibili kwa ajili hiyo tabu nyingi alizozishinda daima kwa imara; akapanga moyoni mwake safari ya roho kulenga ukamilifu wa Kikristo kama kupanda kwa ngazi hadi kwa Mungu; akaandika pia vitabu vyenye mafundisho ya hali ya juu na yaliyotokana na mang'amuzi yake ya dhati[1].

Ni kati ya watu muhimu zaidi katika ya historia ya Kanisa ya karne ya 16, katika historia ya utawa na katika teolojia ya Kiroho kutokana na urekebisho aliouanzisha katika shirika la Wakarmeli (wanawake na wanaume vilevile) na kutokana na maandishi yake juu ya maisha ya kiroho yanayomfanya mwalimu wa sala aliye bora kuliko wote.

Alitangazwa na Papa Paulo V kuwa mwenye heri tarehe 24 Aprili 1614, na Papa Gregori XV kuwa mtakatifu tarehe 12 Machi 1622, na hatimaye na Papa Paulo VI kuwa mwalimu wa Kanisa tarehe 4 Oktoba 1970.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Oktoba[2].

Utoto na ujana

[hariri | hariri chanzo]

Teresa alizaliwa Avila, Hispania, tarehe 28 Machi 1515, katika familia kubwa yenye asili ya Kiyahudi, ikiwa na watoto 9 wa kiume na 4 wa kike.

Akisaidiwa na mfano wa wazazi wake, “waliokuwa waadilifu na wacha Mungu” (alivyosema mwenyewe), tangu utotoni alionekana kuelekea sana maisha ya sala hasa upwekeni.

Kabla ya kufikia umri wa miaka 9 alisoma habari za wafiadini kadhaa ambazo zilimfanya atamani kufia dini hivi kwamba alitoroka nyumbani ili akashiriki kifo chao na kwenda mbinguni. Aliwaambia wazazi wake, “Nataka kumuona Mungu”.

Katika masomo yake ya utotoni aliona njia ya ukweli aliyoijumlisha katika mawazo mawili ya msingi: “Vitu vyote vya ulimwengu huu vitapita”, kumbe Mungu tu ni “wa milele, milele, milele”. Mawazo hayo akaja kuyatumia baadaye katika shairi lake maarufu zaidi: “Usivurugwe na lolote, Usitishwe na lolote, Yote yanapita: Mungu habadiliki kamwe. Subira inapata yote. Aliye na Mungu hakosi kitu; Mungu tu anatosha”. (Shairi, 9)

Alipofikia umri wa miaka 12, alifiwa mama yake, akamuomba Bikira Maria ashike nafasi hiyo.

Akiwa na miaka 13 akatumwa kusomea shule ya bweni ya masista Waaugustino hadi alipoweza kukabili kazi ya kutunza familia ya baba yake.

Vitabu vya kidunia vilikuwa vinamuelekeza kutawanyika, lakini vile vya Kiroho, hasa vya Wafransisko, vilimuingiza katika maisha ya umakinifu na sala.

Mpenzi wa kusoma vitabu vya mababu wa Kanisa, hasa Augustino na Gregori Mkuu, alipata wito wake wa kitawa kwa kusoma vile vya Jeromu.

Miaka ya kwanza monasterini

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1536, akiwa amefikia hakika ya kuitwa utawani, alijiunga na monasteri ingawa kwanza baba yake hakukubali, akajichagulia jina la “Teresa wa Yesu”.

Alipojiunga na monasteri ya Wakarmeli wa mji wake, alikuta juhudi za masista wamonaki zilikuwa za kiasi.

Mwenyewe, kisha kuweka nadhiri zake, aliamua kulenga ukamilifu, lakini kwa kukosa busara katika juhudi zake miaka 3 baadaye aliugua sana, ikambidi baba ampeleke kwa matibabu kwenye mji wa jirani, na hatimaye amrudishe nyumbani ili kusubiri kifo. Monasterini waliandaa kaburi, ila baba alikataa asizikwe.

Kumbe, baada ya siku nne za kupotewa kabisa na ufahamu, alianza kupata nafuu hata akaweza kurudi utawani, ingawa kwa muda fulani alikuwa amepooza tu. Mwenyewe alifananisha hali hiyo ya afya yake na ile ya roho yake kutokana na yeye kukaidi neema nyingi za Mungu.

Hatimaye, alipopona kabisa, alisema ni kwa maombezi ya Mt. Yosefu, ambaye tangu hapo alimheshimu sana.

Mwaka 1543 alipotewa na familia yake: baba alikufa na ndugu zake wote walihamia Amerika, mmoja baada ya mwingine.

Baada ya muda wa ulegevu, alipopoteza muda mwingi sebuleni, bila kujali maonyo ya muungamishi wake, na alipojiona anafanana na Augustino wa Hippo katika mapambano dhidi ya udhaifu wake, katika Kwaresima ya mwaka 1554 aliguswa sana na sanamu iliyomuonyesha Yesu katika uhalisia wa mateso yake. “Ghafla hisi ya uwepo wa Mungu ilinijia, nisiweze kabisa kutia shakani kwamba alikuwa ndani mwangu wala kwamba mimi nilikuwa nimevutwa kabisa ndani Mwake“.

Tangu hapo Teresa alishika maisha magumu kabisa, akijitahidi kujikusanya peke yake mbele ya Mungu.

Baadaye aliishi karibu miaka mitatu katika nyumba ya mwanamke mjane mwenye ibada sana aliyeongozwa na Wajesuiti.

Juhudi kwa ajili ya urekebisho

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1560, pamoja na wenzake wachache, alitambua haja ya kutengeneza upya maisha ya Karmeli, na alijisikia kuitwa na Mungu kuongoza kundi lao, akaanza kazi yake kubwa ya urekebisho wa shirika kwa msaada wa Yohane wa Msalaba upande wa wanaume.

Mwaka 1562, baada ya kushinda shida mbalimbali, kwa msaada wa askofu wa jimbo, Alvaro de Mendoza, alianzisha monasteri ya kwanza ya urekebisho mjini Avila chini ya usimamizi wa Mt. Yosefu. Muda si muda alipata pia kibali cha mkuu wa shirika lote, Yohane Mbatizaji Rossi.

Pamoja na Yohane wa Msalaba mwaka 1568 alianzisha huko Duruelo konventi ya kwanza ya wanaume.

Mwaka 1580 alipata kutoka Roma kibali cha kuunda kanda huru kwa monasteri za urekebisho wake: ndio mwanzo wa shirika la Wakarmeli Peku.

Ingawa alipaswa kusafiri na kushughulika sana ili kuanzisha monasteri nyingine 16 huko na huko, pamoja na kukabiliana na matatizo mengi makubwa, Teresa alifikia vilele vya maisha ya sala na kujaliwa neema nyingi za pekee.

Hiyo inashuhudiwa na maandishi yake, yaliyokusudiwa kufundisha hasa masista wenzake, na ambayo ni kati ya vitabu bora vya Kanisa Katoliki:

Humo inaonekana wazi kwamba juhudi za Kikristo ni hasa kupokea na kuitikia kazi ambayo Roho Mtakatifu anaifanya ndani ya mtu kuanzia ubatizo ili kumlinganisha na Yesu.

Mafundisho yake hayakutokana na vitabu alivyosoma, bali na mang’amuzi yake binafsi pamoja na uchunguzi wa yale ya wengine. Ndiyo maana si ya nadharia tu, bali hasa yanafafanua kinachotokea, yakiingia mpaka ndani ya nafsi.

Maisha yake yalimalizika katika shughuli za kuanzisha monasteri, kwa kuwa alifariki usiku wa kuamkia tarehe 15 Oktoba 1582 huko Alba de Tormes akiwa njiani kurudi Avila baada ya kuanzisha Karmeli ya Burgos. Maneno yake ya mwisho yalikuwa: “Hatimaye ninakufa kama binti wa Kanisa… Saa niliyoitamani imefika, Bwana wangu na Bwanaarusi wangu. Ni wakati wa kukutana na wewe”.

Mafundisho makuu

[hariri | hariri chanzo]

Kama msingi wa maisha yote Teresa alipendekeza maadili ya Injili (kutoambatana na kitu, kupendana, kunyenyekea kwa kupenda ukweli, kuwa na msimamo, kutumaini) bila kusahau maadili ya kiutu (upendevu, usemakweli, utaratibu, adabu, uchangamfu, ujuzi).

Pia alipendekeza usikivu kwa Neno la Mungu na ulinganifu na watu wa Biblia: mwenyewe alijisikia kufanana na Bibiarusi wa Wimbo Ulio Bora, na Mtume Paulo na Kristo katika Mateso na katika Ekaristi.

Alisisitiza hasa umuhimu wa sala ambayo kwake “ni kuhusiana kirafiki na Mungu kwa kuongea mara nyingi kwa siri na yeye ambaye tunajua anatupenda”. Hatua kwa hatua uhusiano huo unastawi na kutawala maisha yote.

Maandishi

[hariri | hariri chanzo]
  • Maisha yake mwenyewe (Autobiografia), yaliyoandikwa mwaka 1565 chini ya padri Pedro Ibáñez, muungamishi wake, ili amuombe Yohane wa Avila aifanyie utambuzi safari yake ya Kiroho; alikiita “kitabu cha rehema za Bwana” kwa kuwa kililenga kuonyesha uwepo na utendaji wa Mungu mwenye huruma katika maisha yake; ndiyo sababu mara nyingi kinaripoti maongezi yake na Bwana katika sala.
  • Safari ya ukamilifu (Camino de perfecciòn), kilichoandikwa mwaka 1566 chini ya muungamishi wake; Teresa alikiita “Maonyo na mashauri ambayo Teresa wa Yesu anawapa dada zake” kwa sababu alikiandika kwa ajili ya wanovisi 12 wa monasteri yake ili kuwahamasisha wawe na maisha ya maadili na ya sala ya dhati kwa ajili ya Kanisa; kati ya sehemu bora za kitabu hicho upo ufafanuzi wa Baba Yetu kama kielelezo cha sala.
  • Jumba la ndani, Makao (Castillo interior, Las Moradas), kitabu chake bora, kilichoandikwa mwaka 1577, ambamo anamfananisha mtu wa sala na jumba lenye vyumba 7 vinavyofikiwa kimoja baada ya kingine kadiri ya maendeleo ya kiroho; ni mtazamo mpya juu ya safari yake mwenyewe lakini pia kinaeleza taratibu za ustawi wa maisha ya Kikristo kuelekea utakatifu chini ya Roho Mtakatifu; vilevile anafananisha badiliko la mtu kutoka maisha ya kawaida hadi yale ya Kimungu na lile la mdudu anayegeuka kipepeo; hatimaye, katika kufafanua hali za juu zaidi, anatumia mfano wa Bwanaarusi na Bibiarusi unaopatikana kwanza katika Biblia.
  • Kitabu cha Monasteri Zilizoanzishwa, alichokiandika katika miaka 1573-1582, kinasimulia maisha ya mwanzo ya urekebisho wake, kikisisitiza nafasi ya Mungu.
  • Ripoti, nyongeza ya kitabu cha maisha yake kwa mtindo wa barua juu ya mang'amuzi yake ya ndani na ya nje.
  • Mawazo ya upendo
  • Mishangao
  • Barua (342 nzima na sehemu 87 za nyingine).

Kulinganisha maandishi yake na yale ya Yohane wa Msalaba

[hariri | hariri chanzo]

Tangu tusome mara ya kwanza maandishi ya Teresa wa Yesu na Yohane wa Msalaba, ni rahisi tutambue tofauti ambazo zimesisitizwa mara nyingi. Zinatokana na tofauti za mitazamo yao.

Teresa alitegemea mang’amuzi yake binafsi, akidokeza neema za pekee alizojaliwa (njozi n.k.) asiwe makini kuzitofautisha na mambo yaliyo ya lazima katika “makao saba” ya jumba la Kiroho. Hivyo alitia maanani kuliko wengine matukio ya kihisi, ya nje na ya ziada yanayoweza yakaendana na sala ya kumiminiwa; vilevile alisisitiza kuzingatia ubinadamu wa Yesu.

Yohane pia alisema kwa mang’amuzi yake binafsi na ya watu aliowaongoza, lakini hakuyataja, akijitahidi kuyachimba kiteolojia, jambo ambalo ni muhimu ili kutofautisha yaliyo ya kawaida na yaliyo ya ziada. Alieleza sababu za hali mbalimbali za sala kwa mafundisho juu ya maadili ya Kimungu na ya vipaji vya Roho Mtakatifu vinavyoendana nayo.

Kwa mtazamo huo alizingatia yaliyo ya lazima katika safari ya kuelekea utakatifu, hasa matakaso ya Kimungu yanayohitajika kwa usafi kamili wa upendo. Hivyo hakuelekea kujali neema za pekee zinazoendana pengine na sala ya kumiminiwa, wala hakusisitiza kuzingatia ubinadamu wa Yesu, akilenga moja kwa moja shabaha kuu ya sala, yaani Mungu aliyemo mwetu, tunayemfikia katika giza la imani kwa njia ya ujuzi ambao anatumiminia na unafanana na mang’amuzi.

Kwa kufanya hivyo amekamilisha maandishi ya Teresa na kutusaidia tuyaelewe.

Hata hivyo, chini ya tofauti hizo kuna msingi mmoja, kwa kuwa Teresa alijua vya kutosha mang’amuzi ya wafuasi wake aweze kuelewa na kueleza nini inatokea kwa kawaida kwa watu wanaopitia hayo makao saba. Tukitumia maelekezo aliyoyatoa huko na huko tunaweza kubainisha zaidi yaliyo ya lazima na yaliyo ya ziada.

Kimsingi watakatifu hao walielewa vilevile sala ya kumiminiwa, muungano na Mungu unaotokana nayo, na matakaso ya Kimungu yanayohitajika ili kuufikia ule kamili.

Ikifaa kuonyesha tofauti zao, inafaa zaidi kuonyesha wanavyolingana na kutambua teolojia inavyoweza kusaidia katika masuala hayo magumu.

Sala zake

[hariri | hariri chanzo]

Bwana wangu, je, hukuweza kujumlisha yote katika neno moja na kusema, “Baba, utupe yote tunayoyahitaji”?

Kwa yule anayejua yote vizuri kabisa, inaonekana haihitajiki zaidi.

Lo, hekima ya milele! Kwako na kwa Baba yako hiyo ingetosha, na kweli ndivyo ulivyosali katika bustani la Getsemane: ulionyesha matakwa na hofu yako, lakini ukajiachilia kwa matakwa yake.

Hata hivyo kwa kuwa unajua hatuko tayari kama wewe, Bwana wangu, kutii matakwa ya Baba yako, ilikubidi ubainishe vizuri maombi, tuweze kuona kama tunayoyaomba yanatufaa, na tujizuie kuomba tukiona haitufai.

Kwa sababu ndivyo tulivyo kwamba, tusipopewa tunayotamani, kwa hiari yetu tunayakataa tunayopewa na Bwana, hata yakiwa mambo bora.

Kwa kuwa hatujioni matajiri mpaka tushike fedha mikononi.


Bwana wangu, kwa hakika saa niliyoitamani sana hatimaye imefika.

Kwa hakika wakati wa sisi kuonana umefika.

Bwana na mwokozi wangu, kwa hakika huu ni wakati wa mimi kuchukuliwa kutoka uhamisho huu niwe nawe milele.

Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.

Usinitenge na uso wako, wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  • "The Delighted Angel" drama about Teresa of Ávila and Rabija al-Adavija by Dževad Karahasan, Vienna-Salzburg-Klagenfurt, ARBOS 1995.
  • "The Interior Castle (Edited by E. Allison Peers)," Doubleday, 1972. ISBN 978-0-385-03643-6
  • "The Way of Perfection (Translated and Edited by E. Allison Peers)," Doubleday, 1991. ISBN 978-0-385-06539-9
  • "The Life of Teresa of Jesus: The Autobiography of Teresa of Avila (Translated by E. Allison Peers)," Doubleday, 1991. ISBN 978-0-385-01109-9
  • "Teresa of Avila: An Extraordinary Life", Shirley du Boulay, Bluebridge, 1995 ISBN 978-0-9742405-2-7
  • "Teresa: Outstanding Christian Thinkers," Rowan Williams, Continuum, 1991. ISBN 0-8264-5081-4
  • "The Eagle and the Dove" Saint Teresa of Avila and Saint Thérèse of Lisieux. by Vita Sackville-West. First published in 1943 by Michael Joseph LTD, 26 Bloomsbury Street, London, W.C.1

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]