Angakusi

Dunia jinsi inavyojizungusha angani.
(Picha hii ina kosa dogo, ikionyesha ikweta ya anga mno upande wa kaskazini)
Angakusi jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji aliyeko kwenye ncha ya kusini.

Angakusi (anga ya kusini, kwa Kiingereza southern sky) ni sehemu za anga zinazoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kusini ya Dunia yetu. Ufafanuzi wake ni "sehemu ya anga upande wa kusini wa ikweta ya anga".

Iko kinyume cha angakaskazi.

Angakusi, angakaskazi

[hariri | hariri chanzo]

Kusudi la kugawa anga nusu mbili za kusini na kaskazini ni tofauti kati ya nyota zinazoonekana kwa mtazamaji akiwa kwenye upande wa kusini au upande wa kaskazini wa Dunia. Tofauti hii huwa kubwa zaidi kadri mtazamaji yupo karibu na ncha za Dunia. Tofauti inapungua kadri mtazamaji yuko karibu na ikweta.

Mtu anayeangalia nyota akiwa upande wa kusini wa ikweta ya Dunia hawezi kuona sehemu za nyota zote zinazoonekana vema upande wa kaskazini. Kwa hiyo hawezi kuona kamwe nyota ya Kutubu (Polaris) iliyopo kwenye ncha-anga ya kaskazini. Kinyume chake watu wengi waliopo Ulaya au Marekani hawawezi kuona kamwe kundinyota la Salibu (Southern Cross)

Mtazamaji aliyeko Afrika ya Mashariki yupo karibu na ikweta, kwa hiyo anaweza kuona nyota nyingi za sehemu mbili zote za anga. Hata hivyo Kutubu haionekani Tanzania (iliyopo upande wa kusini wa ikweta) ikiweza kutazamwa kaskazini mwa Kenya.

Tabia za angakusi

[hariri | hariri chanzo]

Katika mazingira yasiyo na machafuko ya hewa (ukungu, vumbi) au machafuko ya nuru kuna takriban nyota 2000 zinazoonekana vema kwa macho matupu. Mjini penye mianga mingi idadi inapungua kuwa 500 - 100 pekee.

Nyota angavu zaidi ni Shira (Sirius) yenye uangavu wa mag -1.5 iliyopo katika umbali wa miakanuru 8 ikifuatwa na Suheli (Canopus) yenye mag -0.74 na Rijili Kantori (α Centauri) yenye mag 0. Ilhali angakaskazi ina nyota angavu ya Kutubu kama "nyota ya ncha" upande wa angakusi hakuna nyota ya ncha iliyo angavu kweli; Sigma Octantis (σ Oct) kwenye Thumni iliyopo karibu na ncha-anga ya kusini ina mag 5.7 pekee kwa hiyo ni vigumu kuiona kwa macho matupu.

Nyota za Salibu zinasaidia kuona upande wa kusini, mstari kati ya nyota zake za Alfa na Gamma unaelekea hadi ncha-anga ya kusini.

Makundinyota yanayoweza kuangaliwa vema kwenye angakusi ni pamoja na Kantarusi (Centaur), Salibu, Nge (Scorpio) na Mkuku (Carina). Kuna pia galaksi ndogo mbili zilizopo karibu nasi ambazo ni Mawingu ya Magellan.

Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Angakusi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.