Ukabu (kundinyota)

Nyota za kundinyota Ukabu (Aquila) katika sehemu yao ya angani

Ukabu (Aquila kwa Kilatini na Kiingereza) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kusini ya dunia yetu.

Mahali pake

[hariri | hariri chanzo]

Ukabu iko kwenye ikweta ya anga jirani na makundinyota Kausi (pia Mshale au Sagittarius) na Jadi (pia: Mbuzi au en:Capricornus)

Ukabu ilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili walioitumia kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[2]

Jina la Ukabu linamaanisha ndege aina ya tai kutokana na neno la Kiarabu العقاب al-ʿuqaab.[3]

Ukabu ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia[4] Jina latokana katika mitholojia ya Ugiriki ya Kale ambako Αετός aetos (tai) alimsaidia mungu mkuu Zeus kushika radi za umeme na kutekeleza shughuli mbalimbali kwa ajili ya miungu.[5]

Nyota angavu zaidi ni α Alfa Aquilae inayojulikana pia kwa jina Altair yenye uangavu unaoonekana wa 0.75 mag ikiwa umbali wa Dunia wa miakanuru 17.[6] .

Kati ya nyota angavu nyingine kuna

  • β Aquilae (Alshain) ambayo ni nyota yenye rangi njano na uangavu wa 3.7 mag ikiwa na umbali wa Dunia wa miakanuru 45.
  • γ Aquilae (Tarazed) ni nyota jitu jekundu yenye uangavu wa 2.7 mag ikiwa umbali wa Dunia wa miakanuru 460.
  • ζ Aquilae ni nyota yenye rangi ya nyeupe-buluu na uangavu wa 3.0 mag ikiwa umbali wa Dunia wa miakanuru 83.
  • η Aquilae ni nyota jitu yenye rangi ya nyeupe-njano na uangavu wa 4.4 mag ikiwa umbali wa Dunia wa miakanuru 1200.
  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Aquila" katika lugha ya Kilatini ni "Aquilae" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Aquilae, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. Hili ni jina lililotumiwa na mabaharia Waswahili walipotafuta njia zao baharini wakati wa usiku, ling. Knappert 1993
  4. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  5. linganisha Allen, Star-Names and their Meanings, uk. 56 f
  6. Ridpath, Ian (2001), Stars and Planets, Illustrated by Wil Tirion (3rd ed.), Princeton University Press, ISBN 0-691-08913-2
  • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 336 ff (online kwenye archive.org)
  • Knappert, Jan, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331


Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ukabu (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.