Abakuria

Kundi la densi la Wakuria wakiimba na kucheza kule Kenya.

Abakuria (au Wakurya) ni kabila la watu wanaoishi katika wilaya za Rorya, Tarime na Serengeti kwenye mkoa wa Mara, kaskazini mwa Tanzania, na katika kaunti ya Migori katika sehemu ya kusini mashariki ya Kenya.

Mnamo mwaka 2005, idadi ya Abakuria ilikadiriwa kuwa 690,000, ikiwa ni 430,000 wanaoishi nchini Tanzania na 260,000 nchini Kenya.

Lugha yao ni Kikuria.

Abakuria ni wakulima na wafugaji, huku Abakuria wa nchini Kenya wakiegemea sana kwa kilimo nao wa nchini Tanzania wakiegemea sana ufugaji. Hasa Abakuria walio katika wilaya ya Serengeti wanatambulika kama wafugaji.

Kilimo cha asili walikuwa wanalima ulezi mtama na viazi tu kwa ajili ya kutengeneza Togwa (obosara) na Pombe. Mazao mengine yalianza kulimwa miaka ya 1900 baada ya wajerumani kuhimiza kilimo. Wakurya hawapendi kutawaliwa wala kuonewa hivyo walikuwa na saiga lika ya vijana kwa ajili ya ulinzi na usalama hivyo utumwa haukuwaathiri sana. Ila kwa kupenda kwao vita walijiunga sana na jeshi K.A.R (King African Rifle) kupigana vita ya kwanza na ya pili na ya Uganda.

Abakuria wanafanana na Wakisii wa nchini Kenya kwa lugha na umbile. Wanadhaniwa walikuwa kundi moja hadi waliposhambuliwa vikali na Wamasai mnamo karne ya 19 na kusambaratishwa katika maeneo tofautitofauti.

Utengano huo ulisababisha kuweko kwa lahaja mbili ambazo zinaeleweka na kila kundi.

Abakuria wamegawanyika katika "makabila madogo" au koo kumi na sita, nazo ni: Nyabasi, Bakira, Bairege, Bagumbe (wanaoishi Kenya na Tanzania), Batimbaru, Banyamongo, Bakenye, Basimbiti, Basweta, Barenchoka, Baikoma, Bamerani na mengineyo. Makabila haya madogo yote yapo pia katika kabila la Wakisii nchini Kenya.

Wakurya ni kabila ambalo huona vita kama mchezo na kuua ni kama kucheza tu na usiombe ukutane nao wakiwa na hasira. Ila ni watu wema sana wakati wa amani: usipowachokoza hawana ubaya na mtu ila ukiwakosea bila kujua hukusamehe hata kabla hujaomba msamaha ila ukiwakosea makusudi hawana msamaha kabisa. Wakurya ni watu ambao hawasalimu amri ukionesha kuwashinda huenda kujipanga upya na kutafakari ni jinsi gani watashinda na si watu wa kukata tamaa na wakiwa na mori hawaogopi chochote wala lolote wako tayari kukabiliana nalo.

Kabila la Abakuria pia linakaribiana na kabila la Wazanaki katika Mkoa wa Mara nchini Tanzania. Itikadi zao kadhaa zinafanana.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Neno “Kuria/koria”  (Mukuria/Mokoria) etimolojia yake hasa ni kutoka lugha za Kibantu katika lahaja ya Kisimbiti na Kikuria (Kikurya) ambapo neno hilo lilitokana na neno “Okoria” (Okorya) lenye maana ya "Ulaji" ambapo kiasili lilitamkwa “Mokoria” (Mokorya) kwa maana ya “Mle au Mnaokula”. Katika wingi wao jamii ya watu hao ambao hasa ni walaji wakubwa wa nyama waliitwa “Abhakoria/Abhakuria” (Abhakoria/Abhakurya) yaani watu walaji ambapo kutokana na watu hao hapo kale kuwa na  hulka ya kutisha kwa ukali na haiba ya maumbo makubwa ya miili yao, waliitwa “Amakoria/Amakuria” (Makoria/Makuria) ikiwa na maana ya “Majitu”.[1]

Kuanzia karne ya 10 KK hadi karne ya 4 KK Wabantu wa jamii ya Abakuria (Makuria) pamoja na Wasuba kutoka pande za Maziwa Makuu hasa Nyanza (Viktoria Nyanza) walisafiri kupitia mto Nile mweupe hadi Karthoum (Khartoum) na Mashariki ya Kati kufanya kazi za kijeshi kama askari wa kukodiwa katika majeshi ya Waseba wa Kaskazini, Wakushi, Watiro na Waisraeli.[2]

Huko katika Mashariki ya Kati, Wasuba pamoja na Wabantu wa jamii ya “Abakuria” (Makuria) walifika eneo la Mara lenye kuwa na asili ya maji machungu, eneo ambalo kwa lugha ya Kisemitiki katika lahaja ya Kiebrania liliitwa “Mara” maana yake “Machungu”. Maji yenye uchungu yaliyopatikana katika eneo hilo la jagwa katika Mashariki ya Kati  hao Abakuria (Makuria) waliyafananisha na kimiminika kilichotoka kichungu kilichotoka katika utumbo wa  mnyama wa aina ya mbuzi ambao waliuita “Amara” (Mara).

Baada ya kumalizika kwa vita ya Mashariki ya Kati katika karne ya 4 KK, askari hao mamluki wa Kisuba na Kikuria walirudi katika nchi ya Kushi (Bara la Afrika) na kuweka makazi yao katika Nubia (Sudani) katika eneo la “Sobat”. Eneo hilo waliloweka makazi yao liliitwa “Sobat” kutokana na kunasibishwa na jina walilopewa askari hao waliokuwa wakirejea kutoka vitani la “Abasoba” ambalo kwa lugha ya Wabantu wa wakati huo ilimaanisha “Wanaorudi toka vitani au Wanyonyaji”.

Hata hivyo, kutokana na kushamiri kwa vita ya kati ya Warabu na Watu weusi wa pande za Kaskazini mwa bara la Afrika, katika karne ya 15 BK Wabantu hao wa jamii Abakuria (Makuria) walihama na kurejea katika makazi ya mababu wa mbari yao katika eneo la Mara linalopatikana nchini Tanzania ambapo jamii hizo za Wasuba na Wakuria zinaishi kuzunguka ziwa Vikroria katika nchi za Tanzania na Kenya hadi sasa.

Hivyo basi, kutokana na historia ya jamii hii ya Abakuria (Makuria) kuwa watu waaminifu, jasiri na hodari katika medani ya vita, mara tu baada ya uhuru wa iliyokuwa nchi ya Tanganyika katika Afrika ya Mashariki ambayo baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika mwaka 1964 iliitwa Tanzania, Wabantu hao wa jamii ya Abakuria (Makuria) waliendelea kuaminiwa kiasi cha kupewa nafsi za juu katika jeshi la Tanzania.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Maisha Ya Watu Na Wanadamu Anuwai Katika Edeni Ya Tanzania Na Mashariki mwa Dunia, ISBN: 978-9912-40-424-3
  2. Maisha Ya Watu Na Wanadamu Anuwai Katika Edeni Ya Tanzania Na Mashariki mwa Dunia, ISBN:9789912-40-424-3

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Abakuria kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Makala hii kuhusu utamaduni wa Kenya bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Abakuria kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.